Home
Unlabelled
Baada ya Dk. Slaa na Prof. Lipumba, nani wengine dhamira zitawasuta?
“KWANGU mimi kuingia Ikulu ni tunda la lengo kuu ambalo ni
kurudisha maadili ndani ya nchi hii. Nani hajaona matumizi ya rushwa
kwenye mchakato wa Lowassa kutafuta wadhamini? Leo fedha zinazotumika ni
za kina Rostam Aziz – wale wale ambao tukisimama jukwaani tumekuwa
tukiwaita mafisadi. Nimeheshimu na kutii dhamira yangu kwa kuwa naamini
Mungu huzungumza nasi kupitia dhamira zetu” (Dk. Slaa – Agosti 3, 2015).
“Nawaomba radhi sana wanachama na wananchi walioniamini na kuonyesha
mapenzi makubwa kwangu na uongozi wangu. Nimeshiriki vikao vya Ukawa
vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo, dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa
katika uamuzi wetu tumeshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za Taifa za
utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji” (Profesa Lipumba –
Agosti 6, 2015).
Ndugu zangu, nimeshawishika kuanza na nukuu hizo mbili za waliokuwa
vigogo wa Ukawa walioachia nyadhifa zao hivi karibuni kwa kusutwa na
dhamira zao juu ya ujio wa Edward Lowassa katika umoja huo. Namaanisha
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa na aliyekuwa Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Lipumba.
Wote wawili wameziachia nyadhifa zao walizozishika kwa miaka mingi kwa
sababu ya kusutwa na dhamira zao baada ya Ukawa kumpokea Lowassa na
kumteua kuwa mgombea urais wao kupitia Chadema. Ni hatua ambazo
zinathibitisha busara zao, ukomavu wao kisiasa, weledi, uadilifu na
heshima zao kwa umma.
Daima nitawaheshimu watu ambao hupoteza karibu ‘kila kitu’ kwa kujiuzulu
nyadhifa zao za uongozi kwa sababu tu ya kusutwa na dhamira zao. Si
siri kwamba dunia ina watu wachache wenye ujasiri huo wa kutii na
kuheshimu dhamira zao.
Katika andiko lake – A Testament of Hope, mpigania haki za watu weusi wa
zamani wa Marekani, Martin Luther King Jr. anasema hivi: “There comes a
time when one must take a position that is neither safe nor popular but
he must take it because conscience tells him it is right (kuna wakati
ambapo mtu huchukua hatua au msimamo ambao si salama wala unaopendwa
lakini ni lazima auchukue kwa kuwa dhamira inamwelekeza ya kuwa ni kitu
sahihi kukifanya).
Kwa mantiki hiyo, nawapongeza Dk. Slaa na Profesa Lipumba kwa kuketi
chini, kutafakari na kusemezana na nafsi zao, na kisha kufikia hatua ya
kujiuzulu nyadhifa zao kuliko kuendelea na Ukawa ya Edward Lowassa.
Wasingefanya hivyo, dhamira zingeendelea kuwasuta maisha yao yote kwa
sababu walishiriki kueneza imani nchini kuwa ni fisadi. Nawapongeza kwa
kuzishinda roho za kinafiki na za ubinafsi zilizojaa uchu wa pesa na
madaraka.
Kwa hiyo, historia itakuja kuandikwa ya kwamba Dk. Slaa na Profesa
Lipumba waliachia nyadhifa zao baada ya dhamira kuwasuta kwa kushiriki
mchakato wa kumkaribisha Lowassa katika Ukawa, na hata kumfanya mgombea
urais wao. Yaani Lowassa yule yule ambaye kwa miaka kadhaa walikuwa
wakimpigia kelele nchi nzima kuwa ni fisadi! Yaani Lowassa yule yule
aliyeibariki na kuipigia kura ya NDIYO Katiba Pendekezwa inayopingwa na
Ukawa!
Ndiyo maana katika kutafakari hatua yao hiyo ya kijasiri, nimesononeshwa
na lugha aliyoitumia kijana John Mnyika wa Chadema katika kumkosoa
Profesa Lipumba kwa kuchukua hatua aliyoichukua. Mnyika ni kijana mdogo
mno kwa Profesa Lipumba. Mnyika hamkaribii kisiasa, kielimu wala kiumri
Profesa Lipumba, na hivyo alipaswa kumkosoa kiungwana.
Namshauri amsome mwanafalsafa wa zamani wa Ufaransa, Jean-Jacques
Rousseau katika andiko lake kuhusu asili ya kupotea kwa usawa duniani
(Origins of Inequality – page 81 part two). Rousseau anasema hivi:
“Contrary to the law of nature however it may be defined, for a child to
command an old man, for an imbecile to lead a wise man, and for a
handful of people to gorge themselves on superfluities while the
starving multitudes lacks necessities.”
Kwa ufupi anashomaanisha Rousseau, miongoni mwa mambo mengine, ni kwamba
ni kinyume cha sheria ya asili kwa mdogo kumfokea au kumwamrisha
mkubwa. Kosa hilo ni sawa na lile la mjinga kumwongoza mwerevu. Naamini
Mnyika ananielewa, na kama ananielewa, basi naye iko siku dhamira
itamsuta na kumwomba radhi Profesa Lipumba!
Hayo pembeni, turejee kwenye lile suala la kujiuzulu nyadhifa zao kwa
waliokuwa vigogo wa Ukawa – Dk. Slaa na Profesa Lipumba. Hakika,
kuondoka kwao Ukawa kumeibua tafsiri nyingi na mitazamo mingi kwa
Watanzania.
Kuna maswali mengi yanaulizwa mitaani baada ya wiki iliyopita Lipumba
naye kuachia ngazi Ukawa. Baadhi ya maswali hayo ni haya: Inakuaje
Lowassa akimbiwe kule alikokimbilia? Je, nani wengine ndani ya Chadema,
CUF na NCCR wataachia ngazi kwa kusutwa na dhamira zao juu ya suala la
kumpokea Lowassa? Je, kuondoka kwa Slaa na Lipumba kumedhoofisha kiasi
gani kampeni ya Lowassa ya kuusaka urais kupitia Upinzani?
Kwanza, labda nianze kwa kusema ya kwamba kuondoka kwa Dk. Slaa
(Chadema) na baadaye Profesa Lipumba (CUF) kunathibitisha kwamba tangu
mwanzo wawili hao hawakupendezwa na hatua ya Ukawa kumpokea Lowassa na
kumfanya mgombea urais wake kupitia Chadema.
Kama hivyo ndivyo, mtu unaweza kujiuliza ni nani hasa walikuwa vinara wa
kumkaribisha Lowassa Ukawa na hata kwenye majadiliano ya iwapo
aruhusiwe kugombea urais au asiruhusiwe? Hisia za wengi ni kwamba
waliokuwa vinara wa kumkaribisha Lowassa Ukawa ni Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia. Dk. Emmanuel Makaidi
hatajwi kwa sababu chama chake hakina ushawishi wowote mkubwa nchini
japo kimo kwenye Ukawa. Ilivyo hivi sasa, Ukawa imebaki ni ya Mbowe na
Mbatia.
Sasa, baada ya Dk. Slaa na Profesa Lipumba kujiondoa, hao wawili (Mbatia
na Mbowe) ndio watapaswa wazunguke naye mikoani wakati wa kampeni za
urais ili ‘kumsafisha’ dhidi ya tuhuma za ufisadi ambazo zimemwandama
kwa miaka 20.
Ikizingatiwa kwamba Mbowe na Mbatia wanatoka Kaskazini (ni Wachaga)
ambako pia anatoka mgombea urais Lowassa, utakubaliana nami ya kwamba si
watu wanaofaa sana kumpigia kampeni ya urais. Maswali yataulizwa juu ya
u-kaskazini wa hao watatu – Mbowe, Mbatia na Lowassa. Hakika, picha
ingekuwa tofauti kama angekuwemo Lipumba kwenye kampeni.
Lakini pia lipo suala la Mbowe na Mbatia kugombea ubunge kwenye majimbo
yao kule Uchagani. Sioni ni vipi wawili hao wanaweza kuandamana mikoani
na Lowassa muda wote wa kampeni ‘kumsafisha’ badala ya kujipigia wenyewe
kampeni kwenye majimbo yao Uchagani!
Itapaswa wachague moja - kujipigia kampeni majimboni au kuandamana na
Lowassa mikoani kwenye kampeni za urais ili ‘kumsafisha’. Na kama
wataamua kubaki majimboni, ni nani wengine ambao hawagombei ubunge
wataandamana na Lowassa mikoani ‘kumsafisha!? Au itabidi Lowassa
‘ajisafishe’ mwenyewe wakati wa kampeni?
Nasisitiza tena kwamba hali ingekuwa ni tofauti kama Dk. Slaa na Lipumba
wangelikuwa bado ni viongozi wakuu wa Chadema na CUF. Wawili hao
wangeliweza kuifanya vyema kazi hiyo si tu kwa sababu wao hawagombei
ubunge, lakini pia kwa sababu wanafahamika kote nchini na wana uzoefu wa
kampeni za urais kwa kuwa walishawahi kugombea nafasi hiyo.
Ndugu zangu, ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba kujitoa kwa Slaa na
sasa Lipumba ni pigo kubwa kwenye kampeni ya urais ya Edward Lowassa
kupitia Ukawa. Na hiyo inanifanya nizidi kuamini ya kwamba itakuwa
vigumu mno kwa Edward Lowassa kuutwaa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Sote tunajua ya kwamba Lowassa si mzungumzaji mzuri jukwaani na pia afya
yake si nzuri sana. Katika hali hiyo, alihitaji sana msaada wa
wazungumzaji wazuri kama Profesa Lipumba, Dk. Slaa au Mbowe na Mbatia
ambao nimeshasema kuna shaka kama watakuwanaye (Lowassa) muda wote wa
kampeni.
Kuna wasomaji wangu walinitumia meseji eti kwamba umaarufu na utajiri wa
Lowassa vyenyewe ni kampeni tosha ya kumwingiza Ikulu! Kwamba eti
mapesa yake na umaarufu wake vinatosha, na kwamba hahitaji sana kupigiwa
kampeni na watu wengine.
Mimi nakataa. Kama mapesa na umaarufu peke yake vinatosha, mbona mwaka
2010 Godbless Lema alishinda ubunge kwa kumbwaga Dk. Matilda Buriani
ambaye alisaidiwa na Lowassa kwenye kampeni? Kama mapesa na umaarufu tu
vinatosha, mbona hakumwezesha swahiba wake huyo kushinda ubunge?
Lakini pia mbona Lowassa hakufanikiwa kumsaidia mkwewe kumbwaga Joshua
Nassari katika uchaguzi ule mdogo wa Arumeru Mashariki licha kwamba yeye
(Lowassa) aliamua kujitosa mwenyewe kwenye kampeni kumsaidia mkwewe?
Hapana ndugu zangu, umaarufu na utajiri peke yake havitoshi kumfanya mtu
ashinde urais. Yapo mambo mengine mengi ya kuzingatia kama vile
uadilifu, weledi, uchapakazi, maono, itikadi nk. Kama mapesa na umaarufu
vingekuwa pekee yake vinatosha, basi uchaguzi wa mwaka 2010 Chadema
isingeambulia jimbo hata moja mkoani Arusha ambako ndiko ngome kuu ya
Lowassa!
Kwa hiyo, wanaoamini ya kuwa Lowassa atashinda urais kwa sababu tu ni
maarufu na tajiri wanajidanganya. Wanaoamini ya kwamba utajiri na
umaarufu wa Lowassa utawafanya wapiga kura wasahau kabisa tuhuma za
ufisadi zinazomwandama kwa miaka 20, watasononeka ukweli utakapojulikana
Oktoba mwaka huu.
Hao ni wale wale walioamini au walioaminishwa na kina Mbowe kwamba eti
Lowassa akihamia Chadema, basi maelfu ya wanachama wa CCM watamfuata, na
hivyo Chadema itashinda kirahisi Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Mpaka sasa
wiki imeshapita tangu Lowassa ahamie Chadema, na bado hatujayaona hayo
maelfu ya wanachama wa CCM wakimfuata! Hali hii inaififisha ile hoja ya
umaarufu wake iliyotumiwa na Mbowe na wenzake kumsimamisha agombee urais
kupitia Chadema.
Kwa hakika, hata wale waliokuwa maswahiba wake wa karibu katika CCM kama
vile Peter Serukamba, Rostam Aziz, Andrew Chenge, Emmanuel Nchimbi,
Adam Kimbisa, Sophia Simba nk mpaka sasa wameamua kubaki huko huko CCM!
Mbona hawajamfuata Chadema? Katika hali ya kawaida hao si ndo walipaswa
kuwa wa kwanza kutimka naye Chadema kabla hao maelfu wengine
hawajamfuata?
Ndugu zangu, nihitimishe kwa kusisitiza kile nilichokiandika wiki
iliyopita; nacho ni kwamba, kwa kuitosa ajenda ya ufisadi ili kumpokea
Lowassa, Chadema kimeipoteza nguvu yake kuu ambayo kwayo kilipata
umaarufu kilio nao hivi sasa.
Kwa kuwa itakuwa vigumu kwa Chadema kuwaendea wapiga kura mikoani kikiwa
na Lowassa na ajenda hiyo ya ufisadi kibindoni, sioni namna yoyote
kinavyoweza kushinda uchaguzi wa Oktoba hasa baada ya kuwapoteza Slaa na
Lipumba.
Na hapa bado sijaizingatia hoja nyingine kuwa CCM kitaongeza nguvu zake
maradufu kuhakikisha Lowassa hatwai dola - iwe ni kwa kuiba kura au
mizengwe mingine. Kwa maneno mengine, kama kilipanga mkakati wa ‘bao la
mkono’ sasa kinapanga mkakati wa ‘mabao ya mikono’ ili tu kujaribu
kuudhihirishia umma kwamba huyo bwana kisiasa hana nguvu na umaarufu huo
mkubwa anaohusishwa nao.
Kwa ufupi, lilikuwa ni kosa kubwa la kimkakati kwa Chadema kumpokea
Lowassa na kumsimamisha kama mgombea urais wake. Kosa hilo la kina Mbowe
limetukatisha tamaa wengi wetu ambao tuliamini kuwa Chadema ni chama
bora kinachopinga ufisadi kinachostahili kuwa mbadala wa CCM.
CHANZO: Gazeti la RaiaMwema.
Post a Comment