Edward Ngoyai Lowassa.
“Nimetumia muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu ya kisiasa nchini. Ninajua marafiki wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe kauli…
“Nitakuwa mnafiki kujidanganya mimi mwenyewe na Watanzania kwamba bado nina imani na CCM… CCM niliyoiona Dodoma siyo kile chama nilichokulia chenye maadili. Ni dhahiri kuwa CCM kimepotoka na kupoteza maadili.
“Hivyo basi, baada ya kutafakari nimeamua kuanzia leo kuondoka CCM na kujiunga na Chadema kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi yetu,” hiyo ilikuwa ni kauli ya kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Ngoyai Lowassa aliyewahi pia kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kabla ya kuamua kuchukua ‘maamuzi magumu’ ya kujiuzulu wadhifa wake kufuatia sakata la Richmond.
Mshtuko nilioupata jioni ya Jumanne, Julai 28,2015 kumuona Lowassa runingani akikabidhiwa kadi ya Chadema yenye rangi ya bluu, nyekundu na nyeupe badala ya kijani kama ilivyozoeleka, ulinifanya nihisi kuwa labda nipo ndotoni na muda mfupi baadaye nitazinduka.
Haikuwa hivyo, Lowassa alikuwa ameamua kukihama CCM baada ya jina lake kukatwa kwenye mchakato wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho.
Jioni hiyo, Lowassa alieleza mambo mengi lakini kubwa nililoliona, alikuwa amechoshwa na kilichokuwa kinaendelea ndani ya chama chake. Akalalamika sana kwamba amekuwa akihujumiwa mno kwa kipindi kirefu ndani ya chama hicho kilichomlea!
Haikuwa kwangu tu, Watanzania wengi walishtushwa na kushangazwa mno na uamuzi huo wa Lowassa, nchi nzima ikagubikwa na mjadala mkali juu ya uamuzi huo wa Lowassa, kila mtu akazungumza lake lakini mwisho wa siku hakuna aliyeweza kubadilisha ukweli, Lowassa alikuwa amejiunga Ukawa.
Siku chache baadaye, Lowassa akachukua fomu za kugombea urais kupitia Chadema! Mshtuko ukaendelea kutawala kila kona, watu wakawa hawaamini kumsikia Lowassa akiwasalimu wanachama wenzake kwa salamu ya Chadema; “Pipooooz!” Kwa kishindo watu wakajibu: “Pawaaa!”
Ungeweza kudhani ni mchezo wa kuigiza unaendelea lakini hiyo ndiyo hali halisi, tayari Lowassa ameshachukua fomu na anatajwa kuwa ndiye atakayepeperusha bendera ya Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD katika nafasi ya urais.
Lowassa ameweka rekodi, katika historia ya Tanzania, yeye ndiye mwanasiasa wa kwanza aliyefikia ngazi ya uwaziri mkuu kukihama chama tawala na kugombea urais kupitia upinzani.
Utakuwa ni upuuzi kumdharau au kumbeza Lowassa kwamba hawezi kuingia ikulu kwani kabla hajakihama CCM, ilikuwa wazi kwamba ndiye mwanasiasa aliyekuwa akikubalika zaidi ndani ya chama hicho! 
Hata baada ya kuhama, kila mmoja ni shahidi wa jinsi ulimwengu wa siasa ulivyotingishika hapa Tanzania! Lowassa ana nguvu! Lowassa ana wafuasi wengi na hizo ni miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya akavunja rekodi nyingine ya kuingia Ikulu ya Magogoni akitokea upinzani.
Mengi bado yanaendelea kuzungumzwa huko mitaani, wapo wanaowaona Chadema wamelamba matapishi yao kwa kuwa siku za nyuma walikuwa wakimshambulia sana Lowassa kwa tuhuma za ufisadi! Wapo wanaoona kama chama hicho kimekosea sana kumkaribisha lakini ukweli utabaki palepale, Lowassa anagombea urais kupitia Ukawa.
VIA: GLOBAL PUBLISHERS

Post a Comment

Powered by Blogger.