Je unapenda mihogo ? Mie pia napenda sana mihogo, hasa mihogo ya kuchoma, ikiwa na pilipili na kachumbari yenye limao la kutosha. Kuna nini kingine kinaweza kuzidi ladha hii tamu?

Mihogo ni chakula kikuu katika kanda nyingi za nchi za tropiki. Pia, mihogo hustawi vizuri sehemu kame kutokana na kutohitaji maji mengi. Mihogo pia ni chanzo kikubwa cha wanga kwa bei nafuu, hasa kwa nchi za kusini mwa jangwa la sahara. Mihogo hutumika kama chakula – ugali wa muhogo na kutengeneza bidhaa tofautichips, mihogo ya kukaanga, kuchemsha n.k.

Kwa muda mrefu tafiti tofauti zinaonyesha madhara ya mihogo kwa maisha ya walaji wake, hasa wale wasiofanya maandalizi mazuri kabla ya kula chakula hiki. Tafiti zinaoyesha kuwa mihogo ina kemikali mbili aina cyanogenic glucosides, zinazoitwa linamarin na lotaustralin. Hizi kemikali pamoja na kimeng’enyo kinachoitwa linamarase, ambacho hupatikana pia kwenye mihogo, huyeyushwa mwilini na kutengeneza kemikali aina ya Cyanide. Cyanide ni sumu ambayo uwepo wake kwa kiasi kidogo mwilini huweza kuleta madhara makubwa ya afya na hata kusababisha kifo.  

Aina za mihogo


Mihogo inaweza kutengwa kwenye makundi makuu mawili – mihogo mitamu na mihogo michungu. Mihogo mitamu ina kiwango kidogo sana cha kemikali hatarishi za cyanogenic glucosides. Hivyo, mara nyingi haina madhara makubwa kama ikiandaliwa vizuri kabla ya kuliwa.

Mihogo michungu ina kiwango kikubwa cha kemikali za cyanogenic glucosides. Uwingi wa hizi kemikali ndio hufanya mihogo hii kuwa michungu zaidi. Hii ni aina ya mihogo inayohusishwa moja kwa moja na madhara ya afya na vifo vinavyotokana na sumu ya cyanide. Mihogo michungu hustawi zaidi sehemu zilizo kame.

Kiwango cha sumu kwenye mihogo


Kiwango cha sumu kilichopo kwenye mihogo hutofautiana. Mihogo mitamu huweza kutoa kiasi cha miligramu 20 za Cyanide kwa kila kilo 1 ya muhogo mbichi. Mihogo michungu hutoa kiasi zaidi ya mara 50 ya hiki kwa kila kilo ya muhogo mbichi – yaani gramu 1 kwa kila kilo 1 ya muhogo mbichi. Fahamu kuwa, kiasi cha miligramu 25 cha cyanide toka kwenye muhogo mbichi inatosha sana kumuua panya. Uwingi wa sumu hii huweza kumuathiri vibaya sana binadamu kwa kuharibu mfumo wa fahamu na kumpa ugonjwa wa kupooza unaoitwa Konzo.

Watoto wadogo wako kwenye hatari zaidi ya kuathirika na mihogo kuliko watu wazima sababu ya udogo wa miili yao kulinganisha na kiwango cha sumu wanayoweza kula kwenye mihogo. Ni muhimu kuwa makini na kila kitu kinachoweza kupewa mtoto kiandaliwe vizuri, na kupunguza idadi ya vitu vibichi ambavyo mtoto anaweza kula – hasa vyakula vya mizizi kama mihogo.

Jinsi ya kuepuka madhara


Nafahamu wengi tumekulia kwa kula mihogo miaka mingi sana, iwe shule au nyumbani, mibichi au ya kupikwa, kawaida au kama unga. Lakini hizi siyo sababu za kupinga utafiti uliothibitishwa. Ili kuweza kulinda afya zetu, za watoto wetu na wale tunaowapenda, hizi hapa njia chache kati ya nyingi zinazoweza kutumika katika kuandaa mihogo vizuri ili kuzuia madhara ya sumu ya mihogo.

1. Usile migoho mibichi


Kuna baadhi ya watu huamini kuwa kula mihogo mibichi huwaongezea nguvu za kiume. Kuna watu wengi huuza mihogo mibichi barabarani na wengi hununua. Mie binafsi sijathibitisha hilo la nguvu za kiume, lakini kutokana na utafiti huu inaonyesha kuwa mihogo huwa na madhara makubwa zaidi ya kiafya kama ikiliwa mibichi. Hivyo ni vizuri kuzingatia ushauri wa kufuata kanuni bora za kuandaa chakula ili kiwe afya badala ya madhara mwilini.

Kwa mtu mwenye mahitaji ya kuongeza nguvu za kiume kwa kutumia vyakula, kuna makala inayohusiana na hivi vyakula ambavyo ni salama kabisa. Unaweza kusoma hapa.

2. Andaa mihogo vizuri


Jamii tofauti zinazotumia mihogo kama chakula kikuu huelewa umuhimu wa maandalizi bora ya mihogo ili kuepuka madhara yake. Wengi hutumia mbinu za kuloweka, kuanika na kupika kwa muda mrefu kabla ya kuwa tayari kuliwa. Kuloweka mihogo au kuanika juani hufanya sumu iliyomo kuondoka na mihogo kuwa salama kuliwa.

3. Usile Maganda


Kiasi kikubwa sana cha sumu ya mihogo imejaa kwenye maganda. Ulazi wa maganda ya mihogo, kwa binadamu au wanyama, huwa na madhara makubwa au hata kifo. Hakikisha maganda yanatupwa na kukaa mbali na mifugo na watoto ambao wanaweza kula bila kujua.

Post a Comment

Powered by Blogger.