Mastaa wawili wakubwa Afrika Mashariki, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mwandani wake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ wanadaiwa kuangusha bonge la pati yenye kila aina ya viashiria vya ufuska, Risasi Jumamosi limeinyaka.
Pati hiyo ya aina yake ilifanyika ndani ya mjengo wa Diamond (white house) uliopo pande za Madale-Tegeta jijini Dar, usiku wa kuamkia siku ya Sikukuu ya Idd El Hajj (Alhamis iliyopita) na kuhudhuriwa na watu maalum tu, ikiwa ni katika kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Zari.
Chanzo chetu cha kuaminika ambacho kilikuwa miongoni mwa waalikwa kilichoomba hifadhi ya jina kilidai kuwa, siku hiyo ilikuwa ya kipekee kwa mastaa hao licha ya kwamba yaliyofanyika hayakuwa na sura nzuri mbele ya jamii.
POMBE KWA SANA
Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, awali, waalikwa wakiwemo mastaa kadhaa walianza ‘kupiga maji’ kwa staili ya taratibu au mdogomdogo hali iliyowafanya kadiri muda ulivyokuwa ukisonga, ndivyo walivyokuwa ‘wakipendeza’.
“Ilikuwa pati ya kufuru lakini watu walikuwa wachache na maalum, waalikwa walianza kwa kupata vinywaji mbalimbali na wale ambao ni watumiaji wa ‘maji machungu’ nao walipata chansi ya kujisevia walichotaka.
“Kwa kuwa pombe zilikuwa za kumwaga, watu walipombeka sana na ulipoingia usiku mnene, wengi walikuwa chicha,” kilidai chanzo hicho.
MUDA WA KUOGELEA
Ilidaiwa kuwa, wakati wengine wakiendelea kuburudika, baadhi walifikia hatua ya kusaula na kujirusha kwenye ‘swimming pool’ (bwawa la kuogelea) iliyopo nyumbani hapo na kuanza kuogelea na wakati mwingine kucheza muziki.
“Kuna wakati baadhi ya watu walijitoa ufahamu kwa kusaula na kubaki na nguo za kuogelea kisha kuzama kwenye bwawa na kuanza kupiga mbizi.
“Si unajua tena watu walikuwa nusu uchi, halafu baadhi walikuwa bwii, sasa unaweza kuvuta picha kilichokuwa kikiendelea kwenye maji, hata hivyo, ilikuwa full burudani aiseee,” kilitiririka chanzo hicho.
KWA NINI PATI YA UFUSKA?
Kwa mujibu wa chanzo hicho, mambo waliyokuwa wakifanya ndani ya mjengo huo hayakuwa ya kistaarabu kwani kubambiana ilikuwa sehemu ya shughuli hiyo.
“Zari mwenyewe alikuwa ndani ya Swimming Costumes (nguo za kuogelea) na mawifi zake akina Esma na Queen Darleen, Diamond mwenyewe, Shetta na wengine ndani ya maji, wakajiachia kisawasawa huku watu wakiwatazama na muziki wa kufa mtu ukipigwa.
“Lakini wapo baadhi ya wanaume ambao hawakuwa wastaraabu kwani walifanya vitendo ambavyo havikuwa vya kistaarabu tena kwa wanawake ambao siyo wao, ilikuwa na sura f’lani ya ufuska.
“Pia wapo baadhi ambao ni Waislam na usiku ule asubuhi yake ilikuwa Sikukuu ya Idd, sasa kufanya tukio lile kwa wakati ule, kusema kweli halikuwa jambo zuri kiimani hasa kwa familia kama ya Diamond,” kililalama chanzo hicho.
ILIKUWA PATI YA SIRI
Chanzo hicho kiliendelea kunyetisha kwamba, pati hiyo iliyofanyika kwa siri huku mapaparazi wakinyimwa nafasi ya kushuhudia kilichokuwa kikiendelea ndani ya jumba la staa huyo ilihudhuriwa na baadhi ya mastaa wachache wakiwemo Shetta, Queen Darleen, TID, Young Dee, Romy Jones na wengine ambao walikuwa ni maalum.
Habari zinaeleza kuwa, katika pati hiyo, Zari au mama Tiffah alikuwa akitimiza umri wa miaka 35 tangu alipoliona jua.
Post a Comment