Maisha ni matamu na raha ya wanaijua wale wanaofahamu siri za
vyakula. Mie nakudokezea siri mojawapo - chakula bora ni muhimu kwa afya
na furaha yako. Bila chakula bora, hakuna raha katika maisha yako hapa
duniani.
Mie huwa napenda kusisitiza kuwa tunakula ili tuishi, siyo tunaishi ili tule.
Tofauti yake ni kubwa sana, maana wale wanaopenda kuishi ili kula
hufakamia chochote ili mradi kiwe chakula, tofauti na wale wanaoishi ili
kula maana hujali zaidi afya zao kwanza kuliko njaa, utamu au mvuto wa
chakula. Tamaa huwa haiwezi kumfanya asahau vitu muhimu kwenye maisha.
Je wewe uko kwenye kundi gani?
Katika mada yetu ya leo tunaangalia vitu ambavyo kwa namna moja au
nyingine hukupunguzia uhai wako maishani. Hivi ni vyakula ambavyo
vinaweza kukufanya ukapata magonjwa usiyotarajia, mfano saratani (cancer), kisuraki, na magonjwa ya shinikizo la damu au moyo.
1. Soda
Mara nyingi vinywaji visivyo na vilevi vimekuwa havimo kwenye orodha
ya vitu visivyo vya afya. Lakini ukweli ni kwamba, vinywaji vingi sana
vinavyouzwa si vizuri kwa afya yako. Mfano mzuri ni soda. Soda ina
kiwango kikubwa sana cha sukari. Utafiti
umeonyesha kuwa madhara ya soda hayatofautiani na madhara ya kuvuta
sigara. Kiwango cha sukari na madawa yaliyomo kwenye soda hukufanyaa
uzeeke zaidi kwa muda mfupi.
2. Vyakula vya kusindika
Vyakula vingi vya kusindika huweza kukaa muda mrefu kwa kutumia dawa,
sukari, mafuta na chumvi kwa kiwango kikubwa sana. Katika hivi viambato
vyote, hakuna hata kimoja kinachokusaidia mwilini bali ni kukuleta
madhara zaidi. Hivyo, ili kuwa na afya, punguza kula vyakula vya
kusindika, na pendelea kula vyakula asilia, hasa mboga za majani.
3. Nyama (Red meat)
Kwa muda mrefu sana nyama imegundulika kuwa chanzo cha magonjwa sugu
kama magonjwa ya moyo na saratani. Nyama pia siyo nzuri kwa afya sababu
husababisha kuongezeka kwa uzito kupita kiasi kama ikiliwa kwa kiwango
kikubwa sana.
4. Pombe
Pombe haiitaji maelezo mengi. Kila mtu anafahamu madhara yake ya muda
mfupi, ambayo huleta matokeo mabaya zaidi kwa wale watumiaji wa muda
mrefu. Pombe, inayonywewa kwa kiwango kikubwa kila mara, hupunguza sana
urefu wa maisha sababu huharibu chembechembe muhimu mwilini hivyo
kuufanya mwili kukosa kinga, na kudhoofika. Ikifika kiwango hiki inakuwa
rahisi kupata magonjwa, na kutoweza kuwa na kinga ya kutosha kuhimili.
Je unawezaje kulinda afya?
Ni vizuri kujali afya, maana kula bila kujali afya ni kama vile
unatembea barabarani kwa kufumba macho ukitegemea hakuna baya
litakalokutokea. Hivyo basi, ni vizuri ukizingatia haya machache:
- Pendelea vyakula asilia – hasa mboga za majani na nafaka bora
- Tumia matunda zaidi, ni bora kuliko juisi au soda za kununua
- Pendelea kula chakula nyumbani kilichoandaliwa vizuri kwa afya
- Usitumie kilevi, kama huwezi, basi kunywa kiasi, ili usije haribu afya yako
- Pendelea kuangalia kiwango cha virutubisho kwenye kila chakula unachokula
- Hakikisha unakunywa maji kwa kiwango kinachotakiwa
Muone daktari mara kwa mara, ili uweze kupata ushauri wa kitaalamu na matibabu muafaka, kabla tatizo halijawa sugu
Post a Comment