SIKU mbili baada ya mawaziri watano kushindwa katika kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM, waziri mwingine, Gaudentia Kabaka anayeshughulikia Kazi na Ajira, naye amedondoshwa katika jimbo la Tarime Mjini.
Kabaka,
kabla ya kujitosa katika siasa za majimbo, alikuwa mbunge wa muda mrefu
wa viti maalumu. Aidha, katika kura hizo zilizofanyika kote nchini,
zimewaacha katika hali mbaya wabunge wanne, baada ya kushindwa katika
kura za maoni majimboni mwao.
Hao ni Nyambari Nyangwine, Gaudence Kayombo, John Lwanji na Salome Mwambu.
Matokeo
ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini ambako Nyangwine ameanguka,
yamethibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu
Wazazi Wilaya ya Tarime, Mathias Lugola aliyetangaza rasmi matokeo ya
majimbo hayo.
Awali,
matokeo hayo ya kura za maoni yaliahirishwa kutangazwa kutokana na
kuwepo kwa tuhuma za kuwapo kwa wizi wa kura. Kwa jimbo la Tarime Mjini,
Lugola alifafanua kuwa Michael Kembaki ndiye aliyeibuka mshindi kwa
kura 3,908 akifuatiwa na Kabaka aliyepata kura 2,411.
Katika
Jimbo la Tarime Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Christopher Kangoye
ambaye amejaribu zaidi ya mara tatu kuusaka ubunge, lakini bila
mafanikio aliibuka mshindi akivuna kura 15,928 dhidi ya 12,205 za John
Gimunta ambaye ni Mweka Hazina wa CCM wilayani Tarime.
Nyangwine na Gimunta, baadaye walilalamikia matokeo hayo wakisema mchakato wa kura za maoni ulitawaliwa na hujuma.
Kayombo azidiwa Mbinga
Katika
Jimbo la Mbinga Vijijini, matokeo yaliyotangazwa saa 5:45 usiku baada
ya mvutano wa kutangaza matokeo unaodaiwa kudumu kwa takribani saa 12,
yameonesha kuwa mbunge wa jimbo hilo aliyekuwa amejitokeza kutetea kiti
chake, Gaudence Kayombo ameshindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.
Aliyeibuka
mshindi ni Martin Msuha, aliyepata kura 13,354 dhidi ya 12,068 za
Kayombo, ambaye pia kwa mwaka mmoja na nusu kati ya Januari 12, 2007 na
Agosti 2, 2008 alikuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.
Wengine
walioshiriki katika mchakato wa ubunge jimboni humo na kura zao kwenye
mabano ni Humphrey Kisika (545), Dk Silverius Komba (1,289), Edesius
Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941) na
Deodatus Ndunguru.
Wabunge Singida hoi
MCHUANO
wa makada mbalimbali wa CCM kuwania nafasi za ubunge katika mkoa wa
Singida umekamilika, huku wabunge waliokuwa wakitetea nafasi zao na
baadhi ya vigogo kwenye chama hicho wakiwa wamebwaga vibaya.
Kwa
mujibu wa Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Mary Maziku, wabunge
wawili waliokuwa wakitetea nafasi zao hawakuweza kupata kura za kutosha
kwenye kura za maoni. Nao ni Salome Mwambu wa Jimbo la Mkalama na John
Lwanji wa Manyoni Magharibi.
Post a Comment